CHAMA cha Wasioona Tanzania (TLB) Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam kimeishukuru Nyumba SACCOS Ltd kwa kuguswa na mahitaji yao, hivyo kuwawezesha kiasi cha fedha na fimbo za kutembelea. Pongezi hizo wamezitoa leo Juni 18, 2022 wakati uongozi wa Nyumba SACCOS Ltd ulipofanya ziara katika ofisi ya chama hicho zilizopo Sabasaba Mbagala kwa ajili ya kukabidhi msaada huo. Katibu wa chama hicho, Wilaya ya Temeke, Bw.Protase Mutakyanga amesema, Nyumba SACCOS Ltd imewapa heshima ya kipekee kupitia msaada wao ambao wameupokea zikiwemo fedha taslimu na fimbo nyeupe.
“Tunawashukuru sana Nyumba Saccos kwa kutupatia fedha kiasi kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kiofisi zikiwemo fimbo 30. Ni jambo la heshima sana, kwa sababu tuliwaomba Nyumba SACCOS fimbo chache,wao wakatuongezea zaidi, kwa kweli tunashukuru sana.
“Huu msaada utatusaidia kwa kiasi kikubwa kutatua baadhi ya changamoto ambazo zinatukabili,pia tunatoa wito kwa wadau wengine ndani ya Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam kuangalia namna ya kujumuika nasi katika masuala mbalimbali yanayotuhusu, sasa tumepata fimbo 30, lakini tuna upungufu wa fimbo 178, hivyo mchango wa wadau ni muhimu sana,”amesema.
Amesema, chama hicho ambacho kwa Wilaya ya Temeke kina wanachama zaidi ya 208 wakiwemo wanaume 127 na wanawake 81 kina mahitaji mbalimbali ikiwemo ofisi, kwa kuwa walipo wanalazimika kupangisha na wakati mwingine huwa wanashindwa kumudu kodi.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Nyumba SACCOS Ltd, Bw.Mwita Bernard Megabe amesema, taasisi hiyo ya hiyari licha ya kuwa na majukumu mbalimbali pia imejiwekea utaratibu wa kugusa maisha ya wengine kulingana na kile kidogo walicho nacho.
Amesema, Nyumba SACCOS licha ya kununua fimbo 30 na kuweka kiasi kidogo cha fedha katika akaunti ya chama hicho, wanaamini kadri njia na fursa zitakavyofunguka nao wataendelea kuyashika mkono makundi mbalimbali mkono kikiwemo chama hicho.